13 July 2009

President Obama’s Responses to SMS Questions (Swahili)

Podcast features questions submitted by and selected by Africans

 

(begin transcript)

RAIS OBAMA:

Afrika ni muhimu kwa maslahi ya usalama wetu.   Kwa hivyo tuliwaomba watu  kutoka kote Afrika watoe maswali yao juu ya kipaumbele cha sera za serikali yangu kuhusu Afrika.

Mamia ya watu walituma maswali kwa maandishi, kupitia Twitter, kwa barua pepe, na kupitia mitandao mingine yo ya kijamii.

Tuliomba jopo la waandishi wa habari wa Kiafrika waliopo Washington wanichagulie maswali matatu ambayo nitayajibu.

Nawashukuru nyote mliotuma maswali.

Swali la kwanza lilichaguliwa na Angela Quintal wa Independent Newspapers,

Pretoria, Afrika Kusini.

Bwana Rais,

Pongezi na karibu Afrika. Mheshimiwa, una mpango gani wa kuwashawishi

Waafrika ambao wamekuwa na ufanisi kote duniani warudi nyumbani na kuchangia ustawi wa Afrika kiuchumi, kisiasa na kadhalika?

Ahsante.”

Kutoka kwa Prince Samuel Nagana, Abuja Nigeria.

Bwana Samuel, nafikiri kwamba kitu muhimu zaidi ambacho tunaweza kufanya kuwashawishi vijana kurudi Afrika ni kwao kujihisi kwamba wana mustakabali, kwamba wanayo fursa barani Afrika.

Na hapo ndipo masuala ya utawala yanapokuwa muhimu sana. Kwa kusikitisha, vijana wengi mno wanahisi kwamba ama nafasi za kiuchumi zimezibwa au ni haba kwa sababu ya ukweli kwamba huenda wakalazimika kutoa hongo ili kupata kazi, wanaweza kuiona serikali ikibadhiri uchumi au inajiingiza sana katika uchumi huo.  Ikiwa watu wanahisi hivyo – kwamba kuna utawala wa sheria.   Ikiwa watu wanahisi kwamba wanapopata elimu wanaweza kuanzisha biashara au wanaweza kuendelea kiuchumi bila kutegemea uhusiano na wakubwa au kigezo kingine chochote ambacho hakihusiani na ujuzi wao na uwezo, basi nafikiri, watakuwa na shauku ya kuzitafuta fursa hizo popote pale watakapozipata.

Na hata kama  sehemu nyinginezo duniani zina kasoro, ikiwemo nchi yangu, Marekani, nafikiri watu bado wanahisi kuwa fursa ni kubwa zaidi huko kwa sababu ya utawala bora.   Hii ndiyo sababu sera zangu za uhusiano na nchi za kigeni zitasisitiza umuhimu wa utawala bora barani Afrika. Nafikiri tunaweza kupata maendeleo makubwa.

Na nafikiri unaweza kuona mabadiliko ya kutoweka kwa wasomi ambako kumekuwa kikwazo kikubwa katika maendeleo ya Afrika.

Swali la pili lilichaguliwa na Mamadou Thior wa RTS, Dakar, Senegal.

“Bwana Rais, hukuchagua kiholela tu kutembelea Ghana.

Nchi hii bila shaka ni mfano mzuri na hata wenye fahari tunapozungumzia demokrasia barani Afrika.  Unafikiri demokrasia ni changamoto ambayo Waafrika wanapaswa kushughulikia au ni tabia wanayopaswa kuiga?”

Kutoka Niger.

Nafikiri uko sahihi kabisa. Nilichagua kwenda Ghana hasa kwa sababu ya kazi kubwa ambayo wamefanya katika kuunda demokrasia inayofanya kazi. Rais Mills alichaguliwa katika uchaguzi wa kura za karibu. Lakini yeye kama mshindi, na mpinzani wake walishirikiana, katika kuhamisha madaraka, kutambua uchaguzi,jinsi ambavyo tunataka demokrasia kuendeshwa, bila ghasia, kuheshimu utawala wa kisheria, kuheshimu matokeo ya uchaguzi. Na hii ni mojawapo ya nguvu kubwa za Ghana, kwa sababu unapoweza kuona mabadiliko ya utawala kwa njia za amani, watu wanapojihisi kuwa sauti zao zinasikika, serikali inafanya kazi vizuri zaidi, inakuwa na uhalali mkubwa, sekta ya kibinafsi katika jumuiya ya kiraia inahisi kwamba ina mchango katika kufanikisha mambo.

Kwa hivyo, maendeleo ya Ghana, nafikiri, yamejionyesha kuwa bora kulinganishwa na baadhi ya nchi ambazo hazina taasisi hizi imara za demokrasia.

Ni kitu ambacho nafikiri, tumekiona kote barani Afrika. Unapokuwa na serikali inayofanya kazi ambayo haitokani na ukabila, lakini ambayo msingi wake ni utawala wa kisheria, basi inakuwa na uwezo zaidi wa kupambana na rushwa, watu wanajitoa zaidi kufanikisha mambo na kila mtu anastawi.

Kwa hivyo tunatumaini kwamba Ghana itaendelea kuhudumu kama mfano bora wa demokrasia barani Afrika. Na tunatumaini kwamba mfano huo utaenea barani kote.

Swali la tatu lilichaguliwa na Peter Kimani wa gazeti “The Standard,” Nairobi, Kenya.

“Una mpango gani wa kukuza na kutekeleza biashara kati ya Afrika na Marekani mbali na AGOA?”

Kutoka kwa Silvian Mabea Solusaje wa Afrika Kusini.

Silvian, Nafikiri kwamba mojawapo ya kanuni ambazo nataka kuleta katika uhusiano wa Marekani na Afrika ni kwamba maendeleo ya kiuchumi Afrika hayatatokana tu na kutolewa kwa misaada ya kigeni lakini itatokana na jinsi tunavyojenga uwezo ndani ya Afrika.

Sasa, kama nilivyosema awali, sehemu fulani ni juu ya Afrika yenyewe, kuinua utawala bora, kukuza heshima kwa utawala wa kisheria na haki za mali, yote ambayo yanaweza kuwahamasisha vijana wenye  vipawa kuwekeza kama wajasiriamali. Hiyo ndiyo itakayosaidia kubadilisha hali.

Lakini kubadilisha sera zetu za biashara kwa ufanisi kutakuwa muhimu vile vile.

Kwa hivyo nataka kutafuta njia zitakazotuwezesha kupanua uhusiano wa  biashara zaidi baina ya Marekani na nchi za Kiafrika. Tunataka, kila tunapoweza, kutoa kila aina ya nafasi za kuyafikia masoko  ya kimataifa ya Marekani jambo linaloweza kubadilisha hali. Na kwa kiasi ambacho tunaweza kuwekeza katika njia ambazo zitawawezesha watu wa kawaida, wakulima, wafanyibiashara wadogo wadogo waweze kuyafikia masoko hayo katika njia iliyo huru na isiyo na upendeleo. Hiyo ni aina ya miundombinu tunayotaka kuzisaidia nchi zijenge. Tunafikiri tunaweza kufanya hivyo. Tumeona maendeleo katika baadhi ya maeneo. Tunapaswa kuongeza juhudi. Na hicho ni kitu ambacho nimedhamiria kama Rais wa Marekani.

This podcast is produced by the U.S. Department of State’s Bureau of International Information Programs.

(end transcript)

Bookmark with:    What's this?